Saturday, 28 December 2013

UJASIRI NA UTHUBUTU WA ASHA BARAKA KATIKA KUTENGENEZA AJIRA KWA VIJANA



ASHA Baraka ni mwanamke wa mfano wa kuigwa kwa ushujaa na ujasiri wake wa kutosita  kujaribu  jambo lenye manufaa kwake na taifa kwa ujumla.
        Mama Asha Baraka amejitoa kusaidia jamii hususan ya vijana kuwaondoa katika dimbwi la umaskini kwa kuwapa ajira ya kupiga muziki katika bendi yake ya African Stars ‘Twanga Pepeta’.

Asha ni mzaliwa wa mkoa wenye rekodi ya muda mrefu ya kuibua vipaji vya wasanii wa muziki na mpira wa miguu. Mkoa huo ni Kigoma, uliopo magharibi mwa Tanzania.
Ni mama aliyetunukiwa na Mungu vipaji lukuki, vilivyoanza kuonekana tangu akiwa katika shule ya sekondari. Vipaji hivyo vimemuweka katika heshima kubwa kiasi cha kupachikwa hadhi ya kuitwa ‘Iron Lady’.


Moja ya vipaji vyake ni kile cha kuweza kumudu kuongoza pasipo kuteteleka kundi la wanamuziki wasiopungua 45 pasipo kujali jinsia zao.
Miaka ya nyuma haikuwa rahisi kwa mwanamke kupata nafasi ya kuongoza kundi la wanaume. Lakini baada ya mkutano wa kina mama uliofanyika katika mji wa Beijing nchini China, umewafumbua macho na kuwakomboa wanawake na sasa wameweza kupata ujasiri mkubwa, mfano wake ni Asha Baraka.

Akieleza historia ya maisha yake, Asha anasema alizaliwa katika Kijiji cha Mwandiga, kilichopo katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, mkoani Kigoma.
         Masomo yake ya msingi aliyapata katika shule mbili tofauti. Darasa la kwanza hadi la tatu alisoma katika Shule ya Msingi Kipampa iliyopo Ujiji, mjini Kigoma.
         Baba yake mzee Ramadhani Baraka alikuwa daktari, hivyo alihamishwa kwenda kufanya kazi katika hospitali nyingine ya Nguruka, mkoani humo.
         Asha alilazimika kufuatana na wazazi wake kwenda Nguruka, akiwamo mama yake mzazi aliyemtaja kwa jina maarufu la Mama Ali Baraka.
Alisoma katika Shule ya Msingi Nguruka darasa la nne hadi alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ya darasa la saba.

Asha Baraka alikuwa ‘kichwa’ darasani kwani alifaulu vema mtihani huo, akachaguliwa kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora.
Vipaji vyake vilianza kujitokeza akiwa katika shule hiyo wakati alipoanza kucheza mpira wa pete na kikapu. Kwa kipindi kifupi akachaguliwa kuingia katika timu ya shule.
Uhodari na umahiri mkubwa aliokuwa nao katika michezo, baadaye alichaguliwa kuwa mmoja wa wanafunzi waliounda timu ya UMISETA mkoani Tabora.

Asha baadaye alizidisha juhudi katika michezo hiyo hatimaye alichaguliwa kuwakilisha Mkoa wa Tabora, akiwa katika timu ya mpira wa pete.
Licha ya kucheza michezo hiyo, Iron Lady, Asha alikuwa mwanariadha mashuhuri akikimbia mbio za mita 100, na kuwa miongoni mwa wanamichezo bora shuleni hapo.
Alipomaliza masomo ya sekondari mwanzoni mwa miaka ya 1980, alipata ajira katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) katika Idara ya Mauzo na Masoko, jijini Dar es Salaam.

Asha Baraka ni mama mwenye familia ya mume na watoto wawili wa kiume. Anawataja kwa majina kuwa ni Mope mwenye umri wa miaka 18, ambaye anasema amefuata nyayo zake za uchezaji wa mpira wa kikapu. Mope alichaguliwa katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18.
Imani ni mtoto wake mwingine mwenye umri wa miaka 14, ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Bearden Paul, iliyopo Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Mama Asha Baraka licha ya majukumu yake ya kazi katika Shirika la Bima la Taifa, pia alikuwa akijishughulisha na biashara ya muziki akiongoza kundi la vijana walioajiriwa katika bendi ya African Stars ‘ Twanga Pepeta’.

Ikumbukwe kwamba kati ya miaka ya 1970 na 1990 kulikuwa na mipango mizuri ambapo mashirika mengi ya umma yalikuwa na timu za michezo ya mpira wa miguu, wavu, kikapu, pete hadi bendi za muziki wa dansi.

Shirika la Bima la Taifa (NIC) lilikuwa mojawapo ambalo lilikuwa na timu za michezo hiyo, pia ilikuwa na bendi ya muziki wa dansi ya Bima Lee Orchestra. Baadhi ya wanamuziki nguli waliowahi kupiga katika bendi hiyo ya Bima Lee ni pamoja na Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Sddy Sheggy, Shaaban Dede ‘Kamchape’ Mafumu Bilali ‘Bombenga’, Maximilian Bushoke, Joesph Mulenga ‘King Spoiler’ na wengine wengi.
Asha Baraka alikuwa mmoja wa wachezaji wa mpira wa pete na kikapu katika timu ya Bima, pia alichaguliwa katika timu ya wilaya hadi ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Kipaji chake cha kukimbia kilimfikisha kuchaguliwa katika timu ya taifa ya riadha, akikimbia mbio za mita 100, kabla ya kuchujwa wakiwa kambini huko Arusha.
“Siwezi kumsahau Juma Ikangaa ambaye aliniletea viatu mahususi kwa ajili ya kukimbilia (Sparks) kutoka Japan. Kabla ya hapo, nilikuwa ninakimbia nikiwa na viatu vya raba,” anasema Iron Lady.
Asha anaelezea zaidi jinsi alivyokuwa akikimbia akisema: “Nilikuwa navua viatu vya raba wakati wa kukimbia, nikiviona vizito na kuamua kukimbia ‘Pekupeku’ na nilikuwa nashinda.”

Katika mashindano hayo alikuwa na wanariadha wa kike wa timu ya taifa akiwemo Mosi Alli na Nzaeli Kyomo, ambao anasema kwamba walikuwa wakimpa moyo wa kushiriki mashindano hayo.
“Mimi hata kuchaguliwa kwangu kukimbiza Mwenge wa Olympic, hakukufanyika kwa upendeleo. Sifa zangu katika riadha zipo kitaifa…” anajigamba Asha Baraka.
Kama nilivyokujuza hapo awali, Asha ana vipaji vingi vilivyochanganyika na utundu wake wa tangu akiwa mdogo.
Utundu huo ulimfanya kujifunza kisha kujua kuendesha gari akiwa na umri wa miaka 14, wakati huo akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora.
“Hata nilipoajiriwa katika Shirika la Bima, nilikuwa nakuja kazini nikiendesha gari, kiasi kwamba watu wengi wakiwamo wafanyakazi wenzangu walinishangaa kuniona nikiendesha ‘mkoko’…” anatamba Asha Baraka.
Kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu wa kuendesha gari, aliwahi kupata shauku ya kushindana katika mbio za magari hapa nchini.

Kwa masikitiko Asha anasema alikosa gari maalumu la mashindano hayo, licha ya kufanya mazoezi makali akipitia maeneo mbalimbali hadi Chalinze.
“Nilikuwa napenda sana kuendesha gari, nilifanya mazoezi makali ya kushindana nikapitia maeneo mengi hadi Chalinze…”. Anajisifu Asha Baraka.

Pamoja na kukosa gari maalumu la mashindano, Asha alijichomeka katika gari la mmoja wa wasindikizaji wa magari hayo ya mashindano na akaweza kuzunguka kutoka mwanzo hadi mwisho wa mashindano hayo.
Mwaka 2000 Shirika la Bima la Taifa liliwataka waajiriwa wote kuomba kazi upya. Anasema wakati tangazo hilo linatolewa yeye alikuwa nje ya jiji kikazi, lakini aliporejea hakutaka kuendelea na kazi, hivyo akaamua kutoandika barua ya maombi ya kazi hatimaye akacha kazi rasmi 2010.

Haikuwa hali ya kawaida kwa Asha kuacha kazi yake nzuri katika Shirika hilo la Bima la Taifa (NIC), lakini ujasiri wa kuthubutu ndio uliomsukuma hadi kuamua kuacha kazi hiyo na kujikita katika shughuli zake za biashara na siasa.

Ili aweze kufanya kazi zake kwa umakini zaidi, mwishoni mwa mwaka 2000 Asha Baraka akaamumua kwenda ‘kubukua’ zaidi. Hivyo akamuomba mwajiri wake kuchukua likizo ya miaka miwili ya bila malipo. Asha alitamani kutimiza ndoto zake za kujiendeleza kielimu.
Hatimaye Asha akakwea ‘pipa’ kwenda nchini Uingereza na kujiunga na Chuo cha Eveline kilichopo Barabara ya Court, nchini humo.

Akiwa chuoni hapo alisomea masomo ya Uongozi na Biashara pamoja na Computer. Pia aliongeza somo jingine la Promotion. Baadaye akarejea nchini mwaka 2004 akiwa mhitimu wa diploma.
Mafunzo aliyoyapata nchini Uingereza yalimsaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuongoza kwa umakini mkubwa Kampuni yake ya Afican Stars Entertainments Tanzania (ASET) akiwa mkurugenzi.

Asha anasema kwamba anajivunia kuwa karibu na wanamuziki wake wa African Stars, wana ‘Twanga Pepeta’ kwa kuwa anapata muda mwingi wa kuzungumza na kuyaelewa matatizo yanayowakabiri wao binafsi na bendi yao sanjari na kujua mafanikio ya bendi.

Iron Lady, Asha hivi sasa yuko mbali katika masuala ya kisiasa, kwani ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Wilaya mpya ya Uvinza, iliyopo mkoani Kigoma.
Pamoja na mafanikio hayo yote, Asha Baraka ni mama asiyekuwa na majivuno kwa yeyote. Asha ni kawaida yake kujichanganya na watu wa rika na jinsia tofauti katika kubadilishana mawazo.
Asha Baraka anatanabaisha kwamba kabla ya kuwa na Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET), kulikuwa na bendi ya African Stars iliyoanza Julai mosi, 1994, katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.

Baadaye bendi za M.K. Group, M.K. Beats na M.K. Sound zikaanzishwa na kaka yake, Ali Baraka, aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Zambia (Zambia Airways).
Bendi ya M.K. Beats ilipata umaarufu mkubwa katika miaka ya 1980 hadi 1990 wakitamba na mtindo wao wa ‘Tunkunyema’ huku magwiji kina Maliki Star, Bwami Fan Fan, Sisco Lunanga wakinogesha chini ya uongozi wa Mzee Shem Ibrahim Karenga. M.K.Gorup nayo ilitikisa Jiji la Dar es Salaam katika Hoteli ya New Africa ikipiga muziki wake katika mtindo wa ‘Ngulupa’ chini ya uongozi shupavu wa Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’. Baadaye Alli akaacha uongozi kwa nduguze Msilwa Baraka, akawa Mwenyekiti na Asha Baraka, Mkurugenzi Mtendaji.
Kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET) iliasisiwa mwaka 2000 na yeye kuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo.

Anasifia Kampuni ya ASET kuwa ni mithiri ya chuo ambacho kinatengeneza vipaji vya vijana kisha kuwaruhusu kwenda popote wanapohitajika pasipo masharti yoyote.
“Tuna Academy ya kuendeleza vipaji vya vijana, inayoitwa Twanga Pepeta Academy. Vijana hao hupewa nafasi ya kupiga muziki siku za Jumamosi pale Mango Garden kabla ya African Stars wana ‘Twanga Pepeta’ kupanda jukwaani…” anasema mkurugenzi huyo wa ASET.
Itakumbukwa kuwa wasanii lukuki maaraufu wanaotamba hapa nchini katika tasnia ya muziki wamepita Twanga Pepeta na baadhi yao ni kina Alli Choki, Ramadhan Banza ‘Stone’, Rogert Hega ‘Katapila’, Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa dunia’ Adolph Mbinga, Abuu Semhando ’Baba Diana’, Khalid Chuma ‘Chokoraa’, Chalres Gabriel ‘Charlz Baba’ n.k.
Akiyaelezea mafanikio mengine katika kampuni yake anasema ni makubwa sana likiwemo la kutoa ajira kwa wanamuziki wa kuingia na kutoka wapatao 45.

Vilevile Kampuni ya ASET imekwisha kutunukiwa tuzo kibao zikiwemo za Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na ile ya Oman Festival nchini Muscat, ambako kulifanyika maonesho kabambe.

Licha ya kuelimisha na kuburudisha, Kampuni yake ya ASET imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii katika matatizo mbalimbali ya kijamii. Akitolea mfano anasema ASET iliwahi kuandaa onesho maalumu la muziki ambapo pesa zote za kiingilio zilizopatika hapo alizikabidhi kwa mwanamuziki mkongwe Muhidini Maalim Gurumo ambaye hali yake ya kiafya bado ni tete.

Asha Baraka ameweza kuajiri wanamuziki wengi wenye vipaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi hususan kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pasipo ubaguzi wowote. Anachojali yeye ni nidhamu na kazi nzuri ya mwanamuziki husika.

Mwaka 2000 wakati wa shindano la Tanzania Musical Awards, The African Stars Band ilifanikiwa kuwa bendi bora ya mwaka kwa mwaka 2000/2002, ambapo wimbo wa ‘Kisa cha Mpemba’ ukawa ndio wimbo bora namba mbili.

Asha Baraka alimalizia kwa kuwaasa wasanii wote kuzingatia upendo na nidhamu ambayo kwake yeye anaona kuwa ndiyo nguzo muhimu kuelekea katika mafanikio ya msanii yeyote.

0 comments:

Post a Comment