Wednesday 27 November 2013

Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?




Wengi hujiuliza ni kitu gani hasa mtu anachopaswa kuwa nacho kusudi aweze kupata mafanikio hasa ya kiuchumi . Wengine hudhani mtu anatakiwa awe na elimu kubwa sana ndipo aweze kufanikiwa, lakini  siyo kweli, unaweza ukawa na elimu kubwa tu hata hivyo hali yako kiuchumi  bado ikawa siyo nzuri.  Pia sina maana  ukiwa na  elimu kubwa huwezi kufanikiwa la hasha, wapo watu wengi tu na elimu zao wamepata mafanikio makubwao kiuchumi.

Na unaweza  ukafikiri pia labda ukifanya kazi kwa kutumia nguvu nyingi sana huku ukilala masaa machache kwa siku  labda utaweza kupata mafanikio ya haraka kiuchumi lakini hilo nalo wataalamu wanakuambia kwamba siyo kweli. Sasa ni nini hasa kinachotakiwa?  Jibu ni kwamba, mtu anapaswa kuwa na tabia za kijasiriamali. Tabia za kijasiriamali zipo nyingi lakini hapa tutaizungumzia hii moja tu ambayo ni uvumilivu.
Uvumilivu ni ile hali ya kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu ili kutimiza lengo ulilojiwekea pasipo kukaka tamaa  haraka  hata ikiwa  utapita muda mrefu kiasi gani. Watu wenye tabia hii, hufanya kila linalowezekana katika kuhakikisha lengo walilojiwekea linatimia, huchagua lengo moja, hawashiki mawili kwa wakati mmoja, hawachoki njiani na ni wabunifu, wanapoona mbinu ama mkakati fulani hauzai matunda basi hubadilisha na kutumia mbinu nyingine katika kuhakikisha tu lengo walilojiwekea limetimia. Hutumia muda wao mwingi kujifunza na kujaribu ujuzi/stadi mpya.
Mambo mengine unayopaswa kuwa nayo ni  wazo zuri la biashara. Biashara yaweza kuwa ni ya aina yeyote ilimradi inakidhi vigezo vya kuwa biashara inayowezekana na kulipa vizuri. Dira na malengo yako ni lazima pia uweze kuvibainisha waziwazi.

0 comments:

Post a Comment