Wednesday 27 November 2013

Jinsi ya kupata mtaji wa Biashara yako kutoka Benki..!



 
Ijapokuwa kitaalamu inasemekana  kwamba kitu kikubwa wakati wa kuanzisha biashara ni wazo na wala siyo fedha (mtaji), lakini ukweli huu unaweza katika mazingira fulani usiwe na maana sana na mahali pengine ukafanya kazi vizuri tu. Hata kama ungelikuwa ni mjadala umeitishwa mtaani kwa watu wa kawaida, nadhani upande wa wale ambao wangesema bila  pesa huwezi kuanzisha biashara ikafanikiwa wangekuwa wengi kushinda wale wanaosema pesa siyo muhimu sana bali wazo. 
Nasema hivyo kutokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya watu mitaani tatizo lao kubwa utawasikia wakilalamika ni 'mtaji' waliokuwa nao kuwa kidogo, hautoshi.
Hoja kwamba ni lazima uwe na fedha angalao kiasi kidogo inazidi kupata nguvu pale tunaposhuhudia watu wa kawaida wengi siku hizi wakienda kujiunga katika taasisi mbalimbali za mikopo na saccos. Isingelikuwa kama pesa ni muhimu, wangelisumbuka kwenda huko kufanya kitu gani?
Katika mazingira ambayo pesa siyo muhimu bali wazo, ni lazima mtu ukubali kupoteza muda wako mwingi, tena uwe mjasiriamali kwelikweli jambo ambalo watu wengi wa kawaida ambao hawajapata mafunzo ya ujasiriamali ni vigumu kukubaliana na wewe. Vinginevyo basi iwe tu ni bahati yako kupata mafanikio, na hili haliwezi kutokea kwa kila mtu, katika watu mia utakuta labda wawili au watatu. Watu wengi mitaani wanaamini kwamba ikiwa utataka mafanikio ya haraka bila ya kuvuja jasho miaka mingi basi pesa ndiyo kila kitu. 
Lakini ndugu msomaji nisije nikakukatisha tamaa wewe ambaye unaamini pesa siyo muhimu sana, kwani unaweza ukaanza bila hata ya kutumia senti tano lakini mbele ya safari ukahitaji fedha. Nafikiri na hivyo ndivyo watu wengi wanavyofanya, unaisisimua biashara aidha kwa kwenda kukopa ama kukaribisha wabia.
Mada yangu hasa haikuwa hiyo ijapokuwa inaweza ikawa na mahusiano kidogo na ile niliyokuwa nimethamiria kuitoa, swimming in a cool water while you are thirst”
Siku moja nilikuwa nimekaa na jamaa yangu mmoja kwa jina anaitwa  E.Mrema, ni mwenyeji  kutoka kule Mkuu Rombo Kilimanjaro eneo liitwalo Mrere Mashati. Tulikuwa tumekaa eneo moja maarufu jijini wanakouza vinywaji na vywakula vya asili ya makabila mbalimbali. Mazungumzo yetu yalitawaliwa zaidi na maswala ya biashara na hasa katika kipengele cha shida ya mtaji.
Massawe alikuwa akilalamika sana juu ya kukosa mtaji wa maana wa kuendeshea biashara zake. Aliwalaumu sana ngugu zake wenye uwezo kwamba hawataki kumsaidia walao msingi kidogo ili na yeye aweze kuinuka kama wao. Aliendelea kuulaumu mfumo mzima wa benki na taasisi nyinginezo za kifedha akidai kwamba, hizi taasisi ndogo ndogo za fedha  hasa zinazokopesha kwa dhamana ya vikundi vya watu watano, hazisaidii chochote zaidi ya kuzidi kumdidimiza mjasiriamali huku zenyewe zikizidi kunufaika. 
Akitolea mfano alisema kuwa yeye binafsi alijiunga na taasisi moja, sasa imeshapita miaka 10 lakini haoni maendeleo yeyote zaidi ya kila wakati kuwaza marejesho kichwani mwake.  Na isitoshe mmoja wa wanakikundi anapokimbia na mkopo taasisi huwatwisha jukumu la kulipa wanachama wenzake pasipo hata kusaidia kumsaka mhusika. Na inaposhindikana kabisa huangalia wenye akiba kubwa na kuichukua kufidia  marejesho ya huyo aliyekimbia.
Baada ya kumsikiliza kwa muda mrefu, ilifika mahali na mimi nikaanza kumuuliza maswali mawili matatu huku tukiendelea kunywa vinywaji vyetu na kutafuna. Katika majibu yote aliyonipa niligundua vitu viwili, cha kwanza ni kwamba ndugu yangu Massawe kwa muda wote wa miaka 10 alikuwa akikopa mikopo midogomidogo kuanzia elfu 50, mpaka laki tano tu, na aliogopa kukopa zaidi ya hapo akihofia baadaye kuja kushindwa kulipa. 
Pili, Massawe hakuwa na dhamana za uhakika ambazo zingemuwezesha kukopa fedha nyingi kuanzia million moja na zaidi.Taasisi ili ikupe fedha kuanzia milioni moja kwenda juu wanahitaji uwe na hati ya kumiliki kiwanja, nyumba au kadi ya gari.
Alinihakikishia kwamba, hapa Dar es salaam hakuwa anamiliki mali nyingine zaidi ya vitu vyake vya ndani, lakini katika kuendelea kumdodosa, alibainisha kwamba huko kwao Mrere Rombo anamiliki shamba la migomba na mikahaha lenye zaidi ya hekari 5 alilorithishwa na babu yake.
kumbe ulafise intala inini?" nikang’aka kwa kilugha bila kutarajia nikimaanisha, “kumbe una shamba kubwa kiasi hicho !”
“You are swimming in a cool water while you are thirst, come on brother ! acha uduwanzi, hebu kimbia kesho upesi ukaweke dhamana benki wakupe minoti uje ukachakarike!” Nilijikuta nikiendelea kububujikwa na maneno mchanganyiko kwa lugha zote tatu.
Ni watu wengi wamekufa masikini, siyo leo tu, tangu enzi na enzi. Walikufa wakiwa wanamiliki rasilimali nyingi kama mashamba na nyumba, wakawaachia watoto wao, watoto nao hulimalima muda ukiisha nao pia huwaachia tena  watoto wao hivyo hivyo na kuendelea.
Hawajui rasilimali kama hizo wangeweza wakazitumia kama dhamana wakaondokana na umasikini huku zikiendelea kubakia vilevile. Leo hii Kariakoo wenyeji wajanja huwaalika wawekezaji wenye mitaji yao, wanajenga magorofa kwa mikataba, baada ya miaka kadhaa labda tuseme miaka mitano, 10, 15 au zaidi, nyumba na ardhi vinarudi tena kuendelea kuwa mali ya familia.

0 comments:

Post a Comment