Friday 27 December 2013

Namna ya kuwavutia wateja katika biashara yako



Wateja ni msingi wa biashara yoyote duniani, bila wateja wa kuwauzia bidhaa au kutoa huduma bishara haiwezi kuwapo, jiulize kuhusu biashara yako inawezaje kuendelea bila wateja? Wajasiriamali wanahangaika na  biashara kwasababu wanaamini kuna wateja.

Wateja ni kila kitu katika biashara, hospitali, vyuo, hoteli, daladala, magazeti, radio na biashara mbalimbali unazozifahamu zote zinahitaji wateja ili ziweze kuendelea.

Jaribu kujiuliza bila wagonjwa ni kwa namna gani shughuli za hospitali zingeweza kuendelea?

Ukosefu wa uelewa kuhusu wateja ni moja ya sababu zinazofanya biashara zianguke na kufungwa baada ya kuanzishwa. Pamoja na changamoto katika soko bado wajasiriamali wanashindwa kuelewa ni kwa namna gani wanaweza kukidhi mahitaji ya wateja wao.



Ni muhimu kuelewa na kukumbuka kuwa, wewe kama mjasiriamali una wajibu wa kuwatafuta wateja, kuhakikisha wanakuja kwako na si wateja wakutafute wewe. Wapo wajasiriamali baada ya kuanzisha biashara wanakaa kusubiri waje badala ya kuwatafuta.

Tuangalie baadhi ya njia ambazo zinaweza kutumika ili kuwavuta wateja katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na wajasiriamali. Ikumbukwe njia hizi ni baadhi katika nyingi ambazo zinaweza kujenga ufanisi na kuwezesha biashara kusonga mbele.

Njia ya kwanza, jiulize biashara yako iko wapi na kama iko sehemu sahihi? Eneo ambalo biashara ipo ni jambo la msingi sana katika kuwavutia wateja na kujenga ufanisi katika biashara. Kumbuka si kila biashara inafaa kwa kila eneo au kila eneo kwa kila biashara!

Unaweza kulalamika kwamba biashara haifanyi vizuri na mambo hayaendi lakini kumbe mwanzo wa yote ni biashara yenyewe kutokuwa kwenye eneo sahihi, haya ni makosa yanayofanywa na wajasiriamali wengi, ni uchaguzi wa eneo sahihi kwa biashara zao.

Inawezekana upatikanaji wa maeneo ya biashara hasa maeneo mazuri yanahusisha gharama kubwa katika upatikanaji wake, la muhimu la kuangalia na kufanyia kazi ni kufanya tathmini ya uhusiano wa eneo na aina ya biashara unayotegemea kufanya.

Njia ya pili, jiulize walengwa wa bishara uliyoamua kuifanya ni kina nani hasa? Je ni wapita njia? Unapoamua kufanya biashara fikiria pia juu ya walengwa halisi wa biashara husika, ingawa wanaweza kutokea wateja mbalimbali lakini lazima walengwa wawepo.

Elewa wateja ni msingi wa mafanikio katika biashara yako, jiulize wateja wako ni akina nani, nini kitawasukuma kununua kwako, je ni watu wenye uwezo wa fedha kiasi gani, wanatoka wapi, maswali haya na mengine yakupe namna ya ‘kutengeneza’ wateja wako.

Kwa mfano ukienda benki kuna akaunti za aina mbalimbali kutokana na madaraja ya wateja, kwa mfano kuna akaunti za makampuni, akaunti za watoto nakadhalika, ndivyo ambavyo mjasiriamali unakumbushwa kufikiria aina ya wateja wako ungependa wawepo.

Ni muhimu kuwa na mchanganuo wa aina mbalimbali za wateja wanaolengwa na bishara yako.Haiwezekani ‘nguo’ moja ikamtosha kila mtu! Kwa mfano kama umeamua kufungua duka la nguo jiulize walengwa wa bidhaa hizo ni kina nani na utawapataje.

Kumbuka soko ni kubwa sana na wateja ni wengi, lakini mjasiriamali unahitaji kuwaainisha wateja wako katika matabaka kutokana na aidha mila,desturi,uwezo wa kiuchumi, jinsia, elimu, au maeneo wanayotoka.

Njia ya tatu ni muainishao wa bei. Ni muhimu kwa wajasiriamali kupanga bei za bidhaa zao kwa namna ambayo itawaridhisha wateja wao.Pamoja na kuwa na soko la bidhaa zako, yakupasa kuwa na bei zenye kukubalika miongoni mwa wateja wako ili waridhike.

Ni muhimu kuangali uwezo wa kiuchumi wa eneo husika, zipo baadhi ya bidhaa ambazo bei zake zinaeleweka na zipo bidhaa ambazo bei zake hutofautiana kutokana na mahali.Hii yote inatokana na uwiano wa kiuchumi, mila, desturi na tamaduni za jamii.

Kuna changamoto kubwa katika upangaji wa bei za bidhaa, hii ni kwasababu mara nyingi bei huwakilisha aidha gharama za uzalishaji wa biadhaa au thamani ya bidhaa husika. Ni muhimu kwa wajasiriamali kuepuka kujifunga na badala yake wacheze na soko.

Njia ya nne, jiulize nani anaendesha biashara? Wapo wajasiriamali ambao kutokana na kujiingiza katika shughuli mbalimbali huwaweka wafanyakazi ili waendeshe biashara husika, jitahidi wewe mwenyewe uwapo kwani kuna faida nyingi za wewe kuwapo:

Faida ya kwanza, kwa wewe mwenyewe kuwapo itakusaidia kuwafahamu wateja wako na kujua mahitaji yao. Utaweza kufahamu nini wanahitaji ambacho biashara yako haina kwa wakati huo na vile vile utapata wasaa kuwasikiliza na kuweza kujifunza.

Faida ya pili uwapo wako katika biashara utakusaidia kuona namna bora ya kudumisha huduma bora kwa wateja. Kumbuka mteja atakayeridhishwa na bidhaa zako atakuwa balozi wa kuwaambia wengine hivyo kujenga wigo mpana wa wateja wa biashara yako.

Kumbuka uchungu wa biashara yako uko katika nafsi yako na si mtu mwingine, usiwaamini sana wafanyakazi wako, hivyo pamoja na mihangaiko ya hapa na pale jiwekee utaratibu wa wewe mwenyewe kuwapo ili kufahamu changamoto za biashara. 

Uwepo wako katika biashara utakusaidia kufahamu ni bidhaa zipi zinapendelewa na wateja zaidi, na wanakwenda umbali gani kupata bidhaa hizo, wanaishi wapi, wanafanya kazi wapi, na ni wapi hasa hupendelea kupata huduma zao au bidhaa.

Njia ya tano ni kuwafahamu washindani wako. Tafuta namna ya kuwafahamu washindani wako kujua wanafanya nini katika kukidhi mahitaji ya wateja wao, ni muhimu kujifunza mabaya na mzuri ya washindani wako, usiwachukulie washindani wako kama maadui.

Kwa mfano ni muhimu kila mara kujiuliza ni mahali gani kwingine wateja wako wanaweza kununua bidhaa kama unazouza wewe? Kutokana na wateja wengi kupenda unafuu katika bidhaa wanazohitaji nao wamekuwa tayari kwenda popote.

Pamoja na kuwafahamu washindani wako, yakupasa mjasiriamali kuwa na namna itakayokutofautisha na washindani wako. Kuwa mbunifu, tafuta namna ambayo itaweza kukutofautisha na washindani wako hata kama mnauza bidhaa zinazofanana.

Kuna namna mbali mbali ambazo unaweza kujaribu kujitofautisha na washindani kama vile  utoaji wa punguzo la bei kwa wateja wanaonunua bidhaa kwa kiasi kikubwa, utayari wa kupeleka bidhaa hadi eneo husika la mteja  na njia nyingine mbalimbali.

Njia ya sita kumbuka biashara ni matangazo, jiulize unafahamikaje? Tafuta namna mbalimbali zenye gharama nafuu ili kuweza kufikisha ujumbe wa kile unachokifanya. Kwa mfano matumizi ya matangazo madogo madogo katika magazeti yamesaidia wengi.

Njia ya saba, ili kufahamu unapoelekea ni muhimu kujifanyia tathmini. Yafaa kujiuliza maswali kama vile, je una wastani wa wateja wangapi kwa siku, juma, au mwezi?  Je unafikiri kuna mwelekeo wa kupata wateja zaidi kununua bidhaa zako kwa siku zijazo?

Je wateja wako tayari kulipia bidhaa kwa bei uliyopanga? Je ni kwa kiasi gani wateja wako wanaridhishwa nawe? Je mahitaji ya bidhaa unazouza yakoje, je ni ya msingi, lazima au au ya kujifurahisha. Je unaridhishwa kiasi gani na kiwango cha mauzo yako?

Kama ambavyo tumeweza kuona wateja ni msingi wa biashara yoyote duniani, ndugu mjasiriamali hakikisha unajitahidi kufanya unaloweza ili kuweza kubaki na wateja ulio nao, unapofikiria biashara yako fikiria juu ya namna bora ya kukidhi mahitaji ya wateja.

0 comments:

Post a Comment