ASHA Baraka ni
mwanamke wa mfano wa kuigwa kwa ushujaa na ujasiri wake wa kutosita kujaribu jambo lenye manufaa kwake na taifa kwa ujumla.
Mama Asha Baraka
amejitoa kusaidia jamii hususan ya vijana kuwaondoa katika dimbwi la umaskini
kwa kuwapa ajira ya kupiga muziki katika bendi yake ya African Stars ‘Twanga
Pepeta’.
Asha ni mzaliwa wa
mkoa wenye rekodi ya muda mrefu ya kuibua vipaji vya wasanii wa muziki na mpira
wa miguu. Mkoa huo ni Kigoma, uliopo magharibi mwa Tanzania.
Ni mama
aliyetunukiwa na Mungu vipaji lukuki, vilivyoanza kuonekana tangu akiwa katika
shule ya sekondari. Vipaji hivyo vimemuweka katika heshima kubwa kiasi cha
kupachikwa hadhi ya kuitwa ‘Iron Lady’.
Moja ya vipaji vyake
ni kile cha kuweza kumudu kuongoza pasipo kuteteleka kundi la wanamuziki
wasiopungua 45 pasipo kujali jinsia zao.
Miaka ya nyuma
haikuwa rahisi kwa mwanamke kupata nafasi ya kuongoza kundi la wanaume. Lakini
baada ya mkutano wa kina mama uliofanyika katika mji wa Beijing nchini China,
umewafumbua macho na kuwakomboa wanawake na sasa wameweza kupata ujasiri
mkubwa, mfano wake ni Asha Baraka.
Akieleza historia ya
maisha yake, Asha anasema alizaliwa katika Kijiji cha Mwandiga, kilichopo
katika Wilaya ya Kigoma Vijijini, mkoani Kigoma.
Masomo yake ya
msingi aliyapata katika shule mbili tofauti. Darasa la kwanza hadi la tatu
alisoma katika Shule ya Msingi Kipampa iliyopo Ujiji, mjini Kigoma.
Baba yake mzee Ramadhani
Baraka alikuwa daktari, hivyo alihamishwa kwenda kufanya kazi katika hospitali
nyingine ya Nguruka, mkoani humo.
Asha alilazimika
kufuatana na wazazi wake kwenda Nguruka, akiwamo mama yake mzazi aliyemtaja kwa
jina maarufu la Mama Ali Baraka.
Alisoma katika Shule
ya Msingi Nguruka darasa la nne hadi alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya
msingi ya darasa la saba.
Asha Baraka alikuwa
‘kichwa’ darasani kwani alifaulu vema mtihani huo, akachaguliwa kwenda kusoma
katika Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora.
Vipaji vyake
vilianza kujitokeza akiwa katika shule hiyo wakati alipoanza kucheza mpira wa
pete na kikapu. Kwa kipindi kifupi akachaguliwa kuingia katika timu ya shule.
Uhodari na umahiri
mkubwa aliokuwa nao katika michezo, baadaye alichaguliwa kuwa mmoja wa
wanafunzi waliounda timu ya UMISETA mkoani Tabora.
Asha baadaye
alizidisha juhudi katika michezo hiyo hatimaye alichaguliwa kuwakilisha Mkoa wa
Tabora, akiwa katika timu ya mpira wa pete.
Licha ya kucheza
michezo hiyo, Iron Lady, Asha alikuwa mwanariadha mashuhuri akikimbia mbio za
mita 100, na kuwa miongoni mwa wanamichezo bora shuleni hapo.
Alipomaliza masomo
ya sekondari mwanzoni mwa miaka ya 1980, alipata ajira katika Shirika la Bima
la Taifa (NIC) katika Idara ya Mauzo na Masoko, jijini Dar es Salaam.
Asha Baraka ni mama
mwenye familia ya mume na watoto wawili wa kiume. Anawataja kwa majina kuwa ni
Mope mwenye umri wa miaka 18, ambaye anasema amefuata nyayo zake za uchezaji wa
mpira wa kikapu. Mope alichaguliwa katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka
18.
Imani ni mtoto wake
mwingine mwenye umri wa miaka 14, ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya
Sekondari ya Bearden Paul, iliyopo Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Mama Asha Baraka
licha ya majukumu yake ya kazi katika Shirika la Bima la Taifa, pia alikuwa
akijishughulisha na biashara ya muziki akiongoza kundi la vijana walioajiriwa
katika bendi ya African Stars ‘ Twanga Pepeta’.
Ikumbukwe kwamba
kati ya miaka ya 1970 na 1990 kulikuwa na mipango mizuri ambapo mashirika mengi
ya umma yalikuwa na timu za michezo ya mpira wa miguu, wavu, kikapu, pete hadi
bendi za muziki wa dansi.
Shirika la Bima la
Taifa (NIC) lilikuwa mojawapo ambalo lilikuwa na timu za michezo hiyo, pia
ilikuwa na bendi ya muziki wa dansi ya Bima Lee Orchestra. Baadhi ya wanamuziki
nguli waliowahi kupiga katika bendi hiyo ya Bima Lee ni pamoja na Jerry Nashon
‘Dudumizi’, Sddy Sheggy, Shaaban Dede ‘Kamchape’ Mafumu Bilali ‘Bombenga’,
Maximilian Bushoke, Joesph Mulenga ‘King Spoiler’ na wengine wengi.
Asha Baraka alikuwa
mmoja wa wachezaji wa mpira wa pete na kikapu katika timu ya Bima, pia
alichaguliwa katika timu ya wilaya hadi ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Kipaji chake cha
kukimbia kilimfikisha kuchaguliwa katika timu ya taifa ya riadha, akikimbia
mbio za mita 100, kabla ya kuchujwa wakiwa kambini huko Arusha.
“Siwezi kumsahau
Juma Ikangaa ambaye aliniletea viatu mahususi kwa ajili ya kukimbilia (Sparks)
kutoka Japan. Kabla ya hapo, nilikuwa ninakimbia nikiwa na viatu vya raba,”
anasema Iron Lady.
Asha anaelezea zaidi
jinsi alivyokuwa akikimbia akisema: “Nilikuwa navua viatu vya raba wakati wa
kukimbia, nikiviona vizito na kuamua kukimbia ‘Pekupeku’ na nilikuwa nashinda.”
Katika mashindano
hayo alikuwa na wanariadha wa kike wa timu ya taifa akiwemo Mosi Alli na Nzaeli
Kyomo, ambao anasema kwamba walikuwa wakimpa moyo wa kushiriki mashindano hayo.
“Mimi hata
kuchaguliwa kwangu kukimbiza Mwenge wa Olympic, hakukufanyika kwa upendeleo.
Sifa zangu katika riadha zipo kitaifa…” anajigamba Asha Baraka.
Kama nilivyokujuza
hapo awali, Asha ana vipaji vingi vilivyochanganyika na utundu wake wa tangu
akiwa mdogo.
Utundu huo ulimfanya
kujifunza kisha kujua kuendesha gari akiwa na umri wa miaka 14, wakati huo
akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora.
“Hata nilipoajiriwa
katika Shirika la Bima, nilikuwa nakuja kazini nikiendesha gari, kiasi kwamba
watu wengi wakiwamo wafanyakazi wenzangu walinishangaa kuniona nikiendesha
‘mkoko’…” anatamba Asha Baraka.
Kutokana na uzoefu
wake wa muda mrefu wa kuendesha gari, aliwahi kupata shauku ya kushindana
katika mbio za magari hapa nchini.
Kwa masikitiko Asha
anasema alikosa gari maalumu la mashindano hayo, licha ya kufanya mazoezi
makali akipitia maeneo mbalimbali hadi Chalinze.
“Nilikuwa napenda
sana kuendesha gari, nilifanya mazoezi makali ya kushindana nikapitia maeneo
mengi hadi Chalinze…”. Anajisifu Asha Baraka.
Pamoja na kukosa
gari maalumu la mashindano, Asha alijichomeka katika gari la mmoja wa
wasindikizaji wa magari hayo ya mashindano na akaweza kuzunguka kutoka mwanzo
hadi mwisho wa mashindano hayo.
Mwaka 2000 Shirika
la Bima la Taifa liliwataka waajiriwa wote kuomba kazi upya. Anasema wakati
tangazo hilo linatolewa yeye alikuwa nje ya jiji kikazi, lakini aliporejea
hakutaka kuendelea na kazi, hivyo akaamua kutoandika barua ya maombi ya kazi
hatimaye akacha kazi rasmi 2010.
Haikuwa hali ya
kawaida kwa Asha kuacha kazi yake nzuri katika Shirika hilo la Bima la Taifa
(NIC), lakini ujasiri wa kuthubutu ndio uliomsukuma hadi kuamua kuacha kazi
hiyo na kujikita katika shughuli zake za biashara na siasa.
Ili aweze kufanya
kazi zake kwa umakini zaidi, mwishoni mwa mwaka 2000 Asha Baraka akaamumua
kwenda ‘kubukua’ zaidi. Hivyo akamuomba mwajiri wake kuchukua likizo ya miaka
miwili ya bila malipo. Asha alitamani kutimiza ndoto zake za kujiendeleza
kielimu.
Hatimaye Asha
akakwea ‘pipa’ kwenda nchini Uingereza na kujiunga na Chuo cha Eveline
kilichopo Barabara ya Court, nchini humo.
Akiwa chuoni hapo
alisomea masomo ya Uongozi na Biashara pamoja na Computer. Pia aliongeza somo
jingine la Promotion. Baadaye akarejea nchini mwaka 2004 akiwa mhitimu wa
diploma.
Mafunzo aliyoyapata
nchini Uingereza yalimsaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuongoza kwa umakini
mkubwa Kampuni yake ya Afican Stars Entertainments Tanzania (ASET) akiwa
mkurugenzi.
Asha anasema kwamba
anajivunia kuwa karibu na wanamuziki wake wa African Stars, wana ‘Twanga
Pepeta’ kwa kuwa anapata muda mwingi wa kuzungumza na kuyaelewa matatizo
yanayowakabiri wao binafsi na bendi yao sanjari na kujua mafanikio ya bendi.
Iron Lady, Asha hivi
sasa yuko mbali katika masuala ya kisiasa, kwani ni mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Wilaya mpya ya Uvinza, iliyopo mkoani
Kigoma.
Pamoja na mafanikio
hayo yote, Asha Baraka ni mama asiyekuwa na majivuno kwa yeyote. Asha ni
kawaida yake kujichanganya na watu wa rika na jinsia tofauti katika
kubadilishana mawazo.
Asha Baraka
anatanabaisha kwamba kabla ya kuwa na Kampuni ya African Stars Entertainment
Tanzania (ASET), kulikuwa na bendi ya African Stars iliyoanza Julai mosi, 1994,
katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.
Baadaye bendi za
M.K. Group, M.K. Beats na M.K. Sound zikaanzishwa na kaka yake, Ali Baraka,
aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Zambia (Zambia Airways).
Bendi ya M.K. Beats
ilipata umaarufu mkubwa katika miaka ya 1980 hadi 1990 wakitamba na mtindo wao
wa ‘Tunkunyema’ huku magwiji kina Maliki Star, Bwami Fan Fan, Sisco Lunanga
wakinogesha chini ya uongozi wa Mzee Shem Ibrahim Karenga. M.K.Gorup nayo ilitikisa
Jiji la Dar es Salaam katika Hoteli ya New Africa ikipiga muziki wake katika
mtindo wa ‘Ngulupa’ chini ya uongozi shupavu wa Aboubakar Kasongo Mpinda
‘Clayton’. Baadaye Alli akaacha uongozi kwa nduguze Msilwa Baraka, akawa
Mwenyekiti na Asha Baraka, Mkurugenzi Mtendaji.
Kampuni ya African
Stars Entertainment Tanzania (ASET) iliasisiwa mwaka 2000 na yeye kuwa
mkurugenzi wa kampuni hiyo.
Anasifia Kampuni ya
ASET kuwa ni mithiri ya chuo ambacho kinatengeneza vipaji vya vijana kisha
kuwaruhusu kwenda popote wanapohitajika pasipo masharti yoyote.
“Tuna Academy ya
kuendeleza vipaji vya vijana, inayoitwa Twanga Pepeta Academy. Vijana hao
hupewa nafasi ya kupiga muziki siku za Jumamosi pale Mango Garden kabla ya
African Stars wana ‘Twanga Pepeta’ kupanda jukwaani…” anasema mkurugenzi huyo
wa ASET.
Itakumbukwa kuwa
wasanii lukuki maaraufu wanaotamba hapa nchini katika tasnia ya muziki wamepita
Twanga Pepeta na baadhi yao ni kina Alli Choki, Ramadhan Banza ‘Stone’, Rogert
Hega ‘Katapila’, Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa dunia’ Adolph Mbinga, Abuu Semhando
’Baba Diana’, Khalid Chuma ‘Chokoraa’, Chalres Gabriel ‘Charlz Baba’ n.k.
Akiyaelezea
mafanikio mengine katika kampuni yake anasema ni makubwa sana likiwemo la kutoa
ajira kwa wanamuziki wa kuingia na kutoka wapatao 45.
Vilevile Kampuni ya
ASET imekwisha kutunukiwa tuzo kibao zikiwemo za Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC), Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na ile ya Oman Festival
nchini Muscat, ambako kulifanyika maonesho kabambe.
Licha ya kuelimisha
na kuburudisha, Kampuni yake ya ASET imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii
katika matatizo mbalimbali ya kijamii. Akitolea mfano anasema ASET iliwahi
kuandaa onesho maalumu la muziki ambapo pesa zote za kiingilio zilizopatika
hapo alizikabidhi kwa mwanamuziki mkongwe Muhidini Maalim Gurumo ambaye hali
yake ya kiafya bado ni tete.
Asha Baraka ameweza
kuajiri wanamuziki wengi wenye vipaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi
hususan kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pasipo ubaguzi wowote.
Anachojali yeye ni nidhamu na kazi nzuri ya mwanamuziki husika.
Mwaka 2000 wakati wa
shindano la Tanzania Musical Awards, The African Stars Band ilifanikiwa kuwa
bendi bora ya mwaka kwa mwaka 2000/2002, ambapo wimbo wa ‘Kisa cha Mpemba’
ukawa ndio wimbo bora namba mbili.
Asha Baraka
alimalizia kwa kuwaasa wasanii wote kuzingatia upendo na nidhamu ambayo kwake
yeye anaona kuwa ndiyo nguzo muhimu kuelekea katika mafanikio ya msanii yeyote.
0 comments:
Post a Comment