Njia 10 za kutimiza
lengo lako maishani Je,unakabiliwa na ugumu katika kutimiza malengo yako
kimaisha? Bado hutakiwi kukata tamaa hata kidogo.
1.KUWA MAHUSUSI NA
MALENGO YAKO :
Kwanza kabisa katika
kuelekea kutimiza malengo yako, unatakiwa kuwa mahususi na unachokitaka. Lakini
pia, ni lazima ujitengee muda maalum wa lini unatakiwa kutimiza lengo hilo.
Usijiwekee malengo yasiyo na mipaka katika kuyatizimiza. Vinginevyo utaishia
kuwaza kila kukicha. Baada ya hapo, yaandike malengo yako kwenye karatasi, kwa
kufanya hivyo kunakusaidia kujiweka karibu na malengo yako.
2.JIKUMBUSHE MARA KWA MARA:
Hakikisha kuwa kila
siku unajikumbusha juu ya majukumu yako katika kutimiza malengo hayo. Weka
karatasi hiyo mahali ambapo utakuwa unaiona kwa urahisi kila mara. Mfano, iweke
kwenye kioo chumbani mwako kwani ni rahisi kuiona na hali hii itakufanya uzidi
kujikumbusha zaidi nini unatakiwa kufanya. Au unaweza kuiweka kwenye meza yako
unayofanyia kazi kila mara. Kama nilivyosema hapo awali kuwa, kiini hasa katika
kufanya hivi ni kuzidi kujikumbusha juu ya malengo yako kila mara. Ni amini,
hufanya kazi.
3. JIHAMASISHE KUCHUKUA HATUA:
Watu wengi hushindwa kuchukua hatua katika
kutimiza ndoto zao kwa sababu hawahamasiki vya kutosha juu ya malengo yao.
Tafuta vichocheo madhubuti vitakavyokusaidia kuhamasika na kuchukua hatua za
muhimu, ni lazima lengo litimie. Kwa mfano, labda lengo lako ni kuacha uvutaji
wa sigara na binti yako ndiye hamasa kubwa katika hili, mfikirie kila unapokuwa
unataka kuvuta.
4. JIADHIBU UNAPOSHINDWA, NA JIPONGEZE
UNAPOFAULU:
Kila unaposhindwa kuchukua hatua, basi
unapaswa kujiadhibu na jipongeze unapofanikiwa kutimiza kile
ulichojipangia.Hakikisha kuwa kila lengo unalojiwekea ni lazima uwe na mikakati
ya kulitimiza. Kwa upande mwingine, unaweza kujiadhibu kwa kuchelewa hata
kulala kama hujatimiza lengo la siku hiyo. Katika kufanya hivyo utajiwekea
mazoea akilini na mwilini kufanya kazi kutokana na jinsi ulivyolenga au
kupanga.
5. JIONE KAMA UMETIMIZA LENGO LAKO:
Hakikisha kila siku unatumia angalau dakika 15
kufikiri akilini mwako katika mfumo chanya kuwa umeshalitimiza lengo lako. Hili
ni zoezi la muhimu sana katika kuelekea kutimiza malengo yako. Kujiweka kama
umeshatimiza Malengo yako akilini mwako, utakuwa unazidi kujihamasisha na
utakuwa unafikisha ujumbe kwenye ulimwengu wa mafanikio kile unachokitaka
maishani. Watu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali kimaisha, hufanya hivi
kila mara, hutimiza malengo yao akilini kabla ya uhalisia. Hii ni kanuni ya
kitaalamu.
6. CHUKUA ANGALAU
HATUA 1 AU 3 KILA SIKU:
Inashauriwa kuwa,
unapaswa kuchukua angalau hatua moja au tatu kila siku zitakazo kuwezesha
kutimiza malengo yako. Hakuna kitakachotokea kwako kama hutachukua hatua
yoyote. Hapa naomba nieleweke kuwa, hata kama utatumia muda mwingi kiasi gani
kuangalia hiyo karatasi yenye malengo yako kila siku, lakini kama hauchukui
hatua yoyote hakuna kitakachotokea. Kwa hiyo chukua angalau hatua moja au tatu
zitakazo kupeleka katika malengo yako kila siku.
7. JIZATITI KWA WENGINE:
Jaribu kuwaambia baadhi ya watu wako muhimu
juu ya malengo yako. Uko siriazi katika kutimiza malengo yako? Kama ni kweli,
jizatiti juu ya malengo hayo. Mwambie kila mtu juu ya kile unachotaka
kukitimiza maishani mako. Mwambie mke wako juu ya malengo yako, waambie wazazi
wako, waambie rafiki na jamaa zako juu ya malengo yako na lini hasa unapanga
kuyatimiza. Ukifanya hivi, utakuwa huna jinsi zaidi ya kutimiza malengo yako,
maana umewaambia watu wa muhimu sana hivyo kushindwa kwako kutimiza malengo
hayo, ni sawa na kujiletea aibu kubwa. Hivyo utachukua hatua siriazi na
kujiletea matokeo halisi. Lakini naomba nitoe angalizo kuwa, simaanishi kwenda
mitaani na kuanza kuwatangazia watu wote, namaanisha watu muhimu tu.
8. PIMA MATOKEO YAKE
:
Pima na jiwekee
muono juu ya matokeo yako. Kamwe huwezi kujua kama unavuka hatua kuelekea
kwenye lengo lako kama hupimi matokeo ya kile unachokifanya kila siku katika
utendaji wako wa kazi. Kama ukigundua kuwa hauzalishi matokeo unayoyataka, basi
huenda huchukui hatua za kutosha, au mikakati unayoitumia siyo sahihi. Hivyo
unapaswa kubadili mikakati katika kujipatia matokeo unayoyataka. Kama
unazalisha matokeo unayoyataka, basi hongera. Chukua hatua zaidi ili ujipatie
matokeo zaidi.
9. KUWA NA SABABU:
Ni lazima uwe na sababu za kwa nini unataka
kutimiza lengo hilo maishani mwako. Ukiwa na lengo lisilo kuwa na sababu mara
nyingi huwa ni vigumu kulitimiza maana hakuna kitu kinachokusukuma katika
kufanya hivyo. Hakikisha unajikumbusha kila mara akilini mwako kuwa ni kwanini
unataka kutimiza hilo lengo maishani mwako. Sababu yako yakinifu ndani ya moyo
ni chanzo cha hamasa. Mara zote kumbuka hili.
10.JIKUMBUSHE YA
JUU:
Ni muhimu sana kujikumbusha yote uliyoyasoma
hapo juu. Utafiti umaonesha kuwa ukitaka tabia fulani ijekengeke, ni lazima
uifanyie mazoezi kila siku ipitayo angalau ndani ya siku 21mfululizo. Japo siyo
rahisi mwanzoni. Ni kama tu kuhamia mazingira mapya, unaweza kujisikia ugumu
kidogo, lakini muda si mrefu utazoea maana akili yako itakuwa imejikita huko.
Ni sawa na hapa. Fanyia mazoezi tabia njema kila siku kwa muda wa siku 21 na
tabia hiyo itakuwa yako milele. Watu wengi huwa hawajiulizi ni kwa jinsi gani
husugua meno yao kila asubuhi. Unajua ni kwa jinsi gani unasugua meno yako kila
asubuhi? Bila shaka ni vilevile kama kawaida. Hivyo ndivyo ninavyomaanisha
kitabia. Unapoanzisha tabia mpya, utafanya mambo vilevile kila siku. Kwa
kufuata njia zote kumi nilizozianisha hapa chini, naamini kwa nguvu zote kuwa
kutimiza malengo yako haitakuwa tatizo tena. Fanya hivyo kwa dhati na utaona
matokeo ya kushangaza. Naomba niishie hapa kwa leo.
ZINGATIA HAYA. Katika maisha,
hakuna kinachoshindikina kama kweli utaamua kwa dhati kukipata. Kinachochangia
watu wengi kutotimiza kile wanachokitaka maishani, ni kutodhamiria kwa nia na
nguvu zote kufuatilia malengo yao. Lakini pia woga huchangia kwa kiasi kikubwa
sana. Kabiliana na hofu. Tunapokuwa waoga, huwa tuna sizi kiakili, kimwili na
kihisia na hushindwa kabisa kuchukua hatua.
Dah, ahsante kwa ushauri wako mzuri. Nitaufanyia kazi.
ReplyDeleteKaribu tena Bw.Kamotta
Delete