Baada ya kumaliza masomo yako, ajira huchukua
nafasi kubwa ya maisha yako. Pamoja na ukweli kuwa lengo kuu la kuajiriwa ni kuingiza kipato, inakubidi
utafute namna nyingine za ziada za kufurahia ajira yako zaidi ya kusubiri tuu
kupata mshahara mwisho wa mwezi. Mazoea ya kusubiri kufanya kazi kwa ajili ya
mshahara tuu, yanaweza kukufanya ukajihisi kuichoka haraka ajira yako, au
kujikuta usiye na furaha kazini, ukitilia maanani kuna changamoto nyingi za
kifamilia, na kijamii utakazokuwa ukikutana nazo.
Makala hii inachambua fursa 5 ukiacha kupata
mshahara. Fursa hizi 5 zinahusu mambo mengine yatakayokufanya uone ajira yako
ina maana zaidi ya mshahara unaoupata. Inawezekana ajira uliyonayo sasa isiwe
na fursa zote ninazozitaja hapa chini, hata hivyo ni matumaini yangu kuwa
ukitafakari kwa umakini unaweza kuambulia fursa walau moja katika hizi
zinazoelezwa hapa chini:-
1.Kushiriki katika kumiliki asasi husika: Kuna baadhi ya asasi zina sera ya kuruhusu
wafanyakazi kuwa wamiliki wa asasi husika. Pia waweza vutia wamiliki wa asasi
uliyopo kukualika uwe mshirika katika umiliki wa asasi yao, kutoka na ufanisi
wako wa kiwango cha juu na kujitoa kwako kwa asasi husika. Ili kufanikiwa
katika hili, boresha ufanisi wako, jenga mahusiano mazuri na wamiliki, na
ujitoe kwa dhati katika kufanikisha mafanikio endelevu ya asasi unayofanyia
kazi.Kwako ajira iwe zaidi ya mshahara, bali ni namna unavyoijenga asasi
utakayoimiliki hapo baadae.
2.Kujenga mtandao: Unapokuwa umeajiriwa unakutana na watu wa aina nyingi, ukianzia na
wafanyakazi wenzako, wateja wa asasi uliyopo, mabosi wako, na wasambazaji wa
huduma na bidhaa mbalimbali. Katika makundi yote haya ya watu utaweza kupata
wateja wako wa baadae utakapotaka
kujiajiri, pia unapata kujuana na kujenga mtandao wa wasambazaji wa bidhaa na
huduma kwako hapo baadae kama vile watu wa benki, wamiliiki au wafanyakazi wa
vyombo vya habari, n.k. Pia katika kundi hili unaweza kupata washauri –mentors
ambao watakujenga kitaaluma na kuongeza uwezo wako wa kumiliki mambo yako
binafsi. Utaweza pia kupata watu ambao wanaweza kuwa wahisani wako wa baadae au
watu utakaomiliki nao biashara hapo baadae.
3.Kuboresha ujuzi wako: Ajira yako inakupatia fursa ya kupata ufahamu kwa njia ambazo pengine
zingekugharimu sana kama wewe mwenyewe ungekuwa unazilipia. Mfano unaweza kuwa
unapata huduma za internet muda wote uwapo ofisini, unapata nafasi ya mafunzo
mbalimbali kupitia semina, na hata kozi mbalimbali unazolipiwa ukasome. Tumia
vema internet ya ofisi kuongeza pia ujuzi wa mambo mengi ya msingi kielimu na
kifikra, na pia kozi au semina unazoenda ziboreshe ujuzi ambao utaboresha
utendaji wako hapo ofisini ili upate fursa nyingine zaidi zinazokuja na ajira,
lakini pia ujuzi huu utauhitaji utakapokua umejiajiri au umebadili sehemu ya
ajira toka asasi ya sasa kwenda asasi nyingine.
4.Kufanya maandalizi ya kujiajiri: Kuwepo kwako katika ajira ni fursa tosha ya
kujifunza kwa vitendo jinsi asasi zinavyoendeshwa ili utakapokuja kujiajiri
utumie uzoefu na uelewa ulioupata kufanya asasi yako iwe ya mafanikio. Kuna
mapungufu utakayoyaona toka katika asasi uliyopo, na mazuri utakayoweza kuiga.
Mambo ni mengi unayoweza jifunza toka aina ya nyaraka zinazotakiwa katika kuendesha
asasi, jinsi ya kuendesha mikutano mbalimbali ndani ya asasi yako, kanuni na
sera zinazofaa katika kuendesha asasi, hadi katika namna ya kujenga mifumo ya
ufuataliaji wa maendeleo ya asasi yako utakapojiajiri.
5.Kutengeneza jina kwa ajili ya watu wengine: Ufanisi
wako kazini, mahusiano yako bora na bosi wako na wafanyakazi wako, na kwa
kupitia mtandao wako utaweza kuja kusaidia watu wengine kupata kazi kwa
kuwapendekeza kwa mtandao wako au kwa mabosi wako. Na kwakuwa tayari umejijengea heshima na uaminifu
mbele za watu wengine, ni rahisi kusikilizwa hivyo ukaweza kusaidia ndugu zako,
jirani au jamaa mbalimbali kupata ajira kwa mgongo wako.
Hitimisho:
Kuzitambua fursa hizi na kuweza kuzitumia vema kunategemea sana na jinsi wewe
mwenyewe unavyodhibiti mwenendo wako kazini. Je, una mahusiano ya aina gani na
wafanyakazi wenzako, bosi wako, na wateja wa asasi yako ? Je, unabidii kiasi
gani ya kujifunza mambo mapya ukiwa kazini, je una ufanisi wa kiwango cha juu
katika utendaji kazi ? Je, unakabiliana vipi na changamoto unazokumbana nazo?
Je unaheshimu vipi taratibu na sera za asasi uliyopo? Je unajua kiwango gani
cha ufanisi unatazamiwa kuwa nacho hapo kazini kwako ? Je, wajua majukumu yako
na unayatekeleza kwa kiwango gani ? n.k
0 comments:
Post a Comment